Taasisia ya Elimu ya Tanzania (TET) ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyoanzishwa chini ya Sheria Na.13 ya mwaka 1975 (CAP 142 RE 2002). Jukumu lake kuu ni kutafsiri sera za Serikali kuhusu elimu kuwa mitaala, vifaa vya kusaidia mitaala, na programu zinazolenga kuwezesha utoaji wa elimu bora katika ngazi za Awali, Msingi, Sekondari, na Elimu ya Ualimu. Majukumu mahsusi ya TET ni: Kusanifu, kuandaa, na kupitia upya mitaala kwa ngazi za Awali, Msingi, Sekondari, na Elimu ya Ualimu; Kuandaa vifaa vya kusaidia mitaala vikiwemo vitabu, mtaala, na miongozo ya walimu; Kutoa mafunzo ya kazi kwa walimu ili kuwawezesha kutekeleza mtaala kwa ufanisi na kwa tija; na Kufanya utafiti kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na elimu, yakiwemo mchakato wa kufundisha na kujifunza na ubora wa elimu kwa ujumla.