Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ni taasisi ya Umma iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Bunge Na. 13 ya Mwaka 1975 (Marejeo ya 2002). Kuanzia mwaka 2009, TET ilifanywa kuwa Taasisi ya Elimu ya Juu isiyokuwa Chuo Kikuu kupitia usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET) wenye namba REG/040. Taasisi ina jukumu la kutafsiri kwa vitendo Sera za Serikali kuhusu Elimu kwa kubuni mitaala na Programu za elimu zitakazowezesha utoaji wa elimu bora katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu. Majukumu mahsusi ya TET NI: Kubuni, kuandaa na kuboresha Mitaala kwa ngazi za Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimu; Kuandaa vifaa saidizi vya kutekeleza mtaala na kuhakiki ubora wa vifaa vinavyolengwa kutumiwa katika ngazi zilizo chini ya mamlaka yake; Kutoa mafunzo kwa watekelezaji na wasimamizi wa Mitaala; na Kufanya Utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya mitaala, ufundishaji na ujifunzaji na elimu kwa ujumla.