PROGRAMU YA KLIC YAENDELEA KUKUZA USHIRIKIANO WA TANZANIA NA KOREA

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambaye pia ni Mkuza Mitaala Bi. Asia Karo amesema kuwa, nchi ya Tanzania na Korea kusini zimeendelea kushirikiana kukuza elimu kwa masomo ya Sayansi kupitia programu ya KLIC inayotekelezwa nchini Tanzania.
Amesema hayo leo Oktoba 21, 2025 katika shule ya sekondari Pugu ambapo ameambatana na ujumbe kutoka Gwanju Metropolitan Office of Education uliopo jimbo la Gwangju uliokuja na wanafunzi wao, Mkuza Mitaala kutoka TET Bw. Mtewele pamoja na viongozi wa shule ya Pugu.
Akielezea lengo la ujio huo, Bi Asia amesema, programu ya KLIC inalenga kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na Korea kupitia masomo ya sayansi pamoja na michezo ambapo hususan taikondo na sarakasi.
Amesema, Programu ya KLIC inasaidia kuwajengea walimu uwezo juu ya matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji, lakini pia programu hiyo inasaidia kupatikana kwa vifaa vya ujifunzaji kwa wanafunzi.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Pugu Mwl. Patrick Yinza amesema wageni kutoka Korea walioambatana na wanafunzi wao wamekuja wakati sahihi kwani shule hiyo inahamasisha matumizi ya teknolojia kwa wanafunzi katika ujifunzaji na ufundishaji.