Uthibiti Ubora
KITENGO CHA UTHIBITI UBORA
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) hutoa huduma ya uthibiti ubora kupitia Kitengo cha Uthibiti Ubora, kikiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uthibiti Ubora. Kitengo hiki husimamia michakato na mifumo inayotumika kuhakikisha ubora wa vifaa vya kielimu vinavyotakiwa kutumika shuleni kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu ngazi ya Stashahada vinakidhi viwango vya juu vilivyowekwa kulingana na ngazi ya elimu husika. Kitengo cha Uthibiti Ubora hufanya tathmini ya vifaa vya kielimu kwa kuzingatia mambo yafuatayo: Sera ya Elimu na Mitaala inayotumika wakati huo; Usahihi na Ubora wa Maudhui; Ubora, Usahihi na Ufasaha wa Lugha; Ujenzi wa Umahiri kwa kutumia Mbinu sahihi za Ujifunzaji na Ufundishaji; Ubora katika Ubunifu na Mpangilio wa Maudhui unaoleta Mantiki; na Ubora katika Uchapaji. Ithibati ya machapisho hayo hutolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kukidhi vigezo vilivyobainishwa katika miongozo maalumu ya machapisho husika. Miongozo hiyo inaweza kupakuliwa katika menyu ya tovuti hii katika kipengele cha Machapisho halafu Sera na Miongozo.
Uthibiti Ubora wa Machapisho ya TET yakiwemo Mitaala, Mihtasari, Vitabu vya Kiada, Kiongozi cha Mwalimu, Miongozo, Moduli na Machapisho Mengine hupitia hatua mbalimbali ikiwemo: Uandaaji wa dondoo za uandishi (Synopsis), Uandishi wa rasimu ya kwanza, uhariri wa maudhui, uhariri wa lugha, na mchakato wa tathmini (Jopo la Tathmini, Kamati ya Taaluma (KATA), Uhakiki kabla ya Baraza la TET na Jopo la Kamishna linalotoa ithibati kupitia Kamishna wa Elimu).
Vilevile, Uhibiti Ubora wa Machapisho ya Wachapishaji Binafsi yakiwemo Vitabu vya Ziada, Rejea, Fasihi Andishi, Vifaa na Maudhui ya Kielektroniki hufanyika kwa hatua mbalimbali ambazo ni: Uhakiki kabla ya Tathmini, Jopo la Tathmini, Kamati ya Taaluma (KATA), Uhakiki kabla ya Baraza la TET na Jopo la Kamishna linalotoa ithibati kupitia Kamishna wa Elimu. Aidha, moduli zinazoandaliwa na kampuni mbalimbali kwa mafunzo mahususi kwa waalimu husika hupewa barua ya Idhini na Mkurugenzi Mkuu wa TET baada ya kujiridhisha kuwa zimekidhi viwango vinavyotakiwa kabla ya kuruhusiwa kutumika.