TET YAENDELEA KUTOA MAFUNZO KWA WALIMU ILI KUIMARISHA UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeendelea kutoa mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa kwa walimu wa halmashauri za Mkoa wa Kigoma ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi nchini.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayoendelea katika shule ya Sekondari Kigoma yamefunguliwa leo Desemba 15, 2025 na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Angela Katabaro aliyeambatana na mwakilishi wa TAKUKURU na wadau kutoka shirika la Enabel.
Dkt. Katabaro amesema, awamu hii ya pili ya mafunzo kwa walimu imelenga katika masomo ya TEHAMA, Elimu ya Mazingira, na Ufundishaji unaozingatia Uwiano wa Kijinsia, huku awamu ya kwanza ililenga masomo ya Sayansi na Hisabati.
Ameendelea kusisitizakuwa, mafunzo hayo yanakuja katika kipindi muafaka, kwani mitaala iliyoboreshwa iliyoanza kutekelezwa Januari 2024 inamhitaji mwalimu mahiri anayemwezesha mwanafunzi kujenga stadi za karne ya 21, zikiwemo fikra bunifu, utatuzi wa matatizo, mawasiliano, na matumizi sahihi ya teknolojia.
Aidha, Dkt Katabaro amesema, TET imeimarisha mifumo ya ujifunzaji kwa njia ya mtandao kupitia majukwaa kama LMS, OpSchool, TET Soma Kwanza TV na Darasa Janja, kuwataka walimu kutumia kikamilifu fursa hii, hasa katika kuimarisha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
Sambamba na hilo, amebainisha kuwa, TET iko tayari kutoa usaidizi wa kitaalamu wakati wowote kwani mwelekeo wa sasa wa elimu unaweka mkazo katika ufundishaji unaolenga kumjenga mwanafunzi umahiri, badala ya maarifa ya nadharia pekee.
Kwa upande wake mratibu wa mafunzo hao kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam, Dkt.Euginia Kafanabo amesema kuwa mafanoz hayo yakitumika vyema, walimu wataweza kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wengi nchini hasa katika maeneo ya shule ambazo zimekuwa na matokeo mabaya.
Nae, Mwakilishi kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Ibrahim Sadick amesema katika kuimarisha mapambano dhidi ya Rushwa nchini TAKUKURU itaendelea kushirikiana na walimu ili kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu kuhusu madhara ya Rushwa.
Naye Mwakilishi kutoka Enabel, Bw. Robert Kisalama amesema kuwa shirika lake limeona vyema kuwajengeea uwezo walimu ambao ndio nguzo kuu ya kumtenegeneza mwanafunzi shuleni na kuwaomba walimu hao kuyapa umuhimu yote watakayowezeshwa.
Jumla ya walimu 167 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo hayo amabayo yanatolewa na Wataalamu kutoka TET, OWM TAMISEMI wataalamu kutoka chuo cha Ualimu Kasulu, Chuo kikuu cha Dar es salaam.