WIZARA YA ELIMU KUENDELEA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA WAANDISHI BUNIFU
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza Sekta ya elimu kwa kutambua na kuunga mkono juhudi za waandishi bunifu na wachapishaji wa ndani.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Shule Patrick Leana amesema kuwa washindi wa Tuzo ya Taifa ya Uandishi bunifu wameonyesha ubunifu na weledi wa hali ya juu na kwamba zawadi walizopokea ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kukuza maarifa na utamaduni wa kusoma nchini.
Aidha, amewapongeza wachapishaji wa kampuni za ndani kwa kuhakikisha vitabu vinachapishwa na kusambazwa kwa wakati, hatua inayowezesha wanafunzi na jamii kupata rasilimali bora za kujifunza.
"Pamoja na kuwapongeza wachapishaji, nitoe shukrani za dhati kwa kamati ya maandalizi na viongozi wote waliowezesha mchakato wa tuzo kwa mchango wao wa kitaaluma na kujitolea," ameongeza Mkurugenzi Leana.
Amesema kuwa ushiriki wa waandishi kutoka kada mbalimbali na maeneo tofauti, ndani na nje ya nchi, ni ushahidi wa hamasa kubwa ya kitaifa na kimataifa katika kukuza uandishi bunifu.
#KaziNaUtu
#TunasongaMbele
#TabasamuLaUtu