UZINDUZI WA VITABU VYA TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU: HATUA MPYA KUKUZA ELIMU NA VIPAJI VYA NDANI
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Anneth Komba, amesema kuwa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi bunifu ni nyenzo muhimu ya kuibua na kukuza vipaji vya waandishi wa ndani.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Februari 17, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vilivyoshinda tuzo hiyo, ameeleza kuwa mpango huo ni chombo cha kitaifa cha kutambua ubunifu na kuendeleza utamaduni wa Kiswahili kupitia maandiko ya waandishi chipukizi na waliobobea.
Dkt. Komba amebainisha kuwa hatua ya kusambaza vitabu kwa shule zote nchini inalenga kuimarisha utamaduni wa kusoma na kuongeza kiwango cha elimu ambapo jumla ya nakala 120,000 za vitabu vitatu vya riwaya Biarasa, ushairi Mgoma ya Mwere, na hadithi za watoto Maziwa ya Kijiji vimechapishwa na vitasambazwa kwa shule.
Ameongeza kuwa kila Shule itapata kati ya vitabu 8 hadi 10. Vitabu hivyo vitatumika kama rasilimali za maktaba na vinatarajiwa kusomwa na wanafunzi wengi, hatua inayoongeza upatikanaji wa maarifa na kuhamasisha kizazi kipya kupenda kusoma.
Aidha, Dkt. Komba alisema kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya juhudi za kukuza sekta ya uchapishaji nchini kupitia zabuni ya uchapishaji iliyoshirikisha wachapishaji wa ndani.
Amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 100 kilitengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa vitabu bora na kuimarisha uchumi wa maarifa nchini.
#KaziNaUtu
#TunasongaMbele
#TabasamuLaUtu