Mtaala wa Elimu ya Msingi wa Shule Zinazofundisha kwa Lugha ya Kiswahili
Mtaala wa Elimu ya Msingi umeandaliwa katika muktadha wa kuhakikisha utoaji wa elimu inayokidhi mahitaji ya sasa ya Mtanzania na yenye kutoa fursa sawa za kujifunza kwa wanafunzi wote. Mtaala umezingatia masuala mbalimbali ikiwemo stadi za Karne ya 21, kukua kwa Sayansi na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na utandawazi. Unalenga kuhakikisha kuwa Elimu ya Msingi inayotolewa ni bora na wahitimu wake wanakuwa ni wazalendo, wanaojitegemea na wenye uwezo wa kuongea lugha zaidi ya moja. Aidha,Elimu ya Msingi inatarajiwa kutoa wahitimu wenye maarifa na stadi mbalimbali zitakazowawezesha kuchangia katika kuifikisha Tanzania katika uchumi wa viwanda. Mtaala pia unasisitiza utoaji wa elimu jumuishi, yaani elimu inayothamini na kuheshimu uwezo, mahitaji, jinsia na kutambua kwamba wanafunzi wote wanaweza kujifunza na kufanikiwa. Aidha mtaala huu unatarajiwa kukidhi matakwa ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa na kumwandaa mwanafunzi wa Tanzania kuishi katika ulimwengu wenye ushindani.
Mtaala huu umegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu Darasa la I-II. Lengo kuu katika sehemu hii ni kujenga umahiri katika stadi za KKK. Sehemu ya pili inaanzia Darasa la III- VII. Lengo kuu katika sehemu hii ni kumwezesha mwanafunzi kujenga ujuzi katika stadi za KKK pamoja na ujuzi katika stadi nyingine za maisha kupitia masomo ya Maarifa ya Jamii, Stadi za Kazi, Kiswahili, Hesabu, Sayansi na Teknolojia, Uraia na Maadili, Kiingereza na masomo chaguzi ya lugha (Kifaransa na Kiarabu). Inatarajiwa kuwa mtaala huu utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.
1. Mtaala wa Elimu ya Msingi Darasa la I-VII
2. Mtaala Rekebifu wa Elimu ya Msingi kwa Mwanafunzi Mwenye UziwiKutoona Hatua ya I-III