WAJUMBE WA ACA WATEMBELEA SHULE YA BAOBAB
Katibu Mtendaji wa vyama vya Jumuiya za Mitaala barani Afrika (ACA) Dkt.Getrude Namubiru ameungana na washiriki wa Kongamano la Sita la Mitaala Afrika kutembelea Shule za Msingi na Sekondari za BaoBab zilizopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani ili kujionea namna mitaala iliyoboreshwa inavyotelelezwa hasa mkondo wa Amali.
Akizungumza katika tukio hilo leo Septemba 25, 2026, Dkt. Namubiru amesema kuwa imekuwa jambo jema kuweza kuona uhalisia zaidi jù ya utekelezaji wa mitaala na kuwaomba washiriki wote kuweza kujifunza wanaporudi katika nchi zao.
"Nimefurahia kuona namna mitaala hii inavyotekelezwa kwa vitendo hasa katika matumizi ya teknolojia katika kufundishia na kujifunzia na nawapongeza sana kwa juhudi kubwa mnazozifanya" amesema Dkt. Namubiru.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba aliweza kufanya wasilisho la Mtaala wa Sekondari ulioboreshwa na namna wanafunzi wanavyogawanyika katika mikondo ya Jumla na Amali.
Dkt.Komba aliwaeleza washiriki hao namna wanafunzi wanaosoma Mkondo wa Amali wanavyoweza kujiingizia kipato wakati wa likizo zao wanapokuwa wakitumia ujuzi wao kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo huviuza.
Naye Mkurugenzi wa Shule za Baobab, Bi.Shani Swai amesema kuwa ni jambo jema kwao kuweza kupata ugeni wa aina hiyo kutoka nchi za Afrika ambapo ameeleza anaamini wameweza kujionea na kujifunza kutokana na yote waliyoyaandaa.
Katika ziara hiyo, washiriki wa ACA walipata fursa ya kuona shughuli mbalimbali za wanafunzi wanazozifanya katika eneo la ujifunzaji kwa vitendo.