TET NA ROOM TO READ ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO KATIKA KUBORESHA MKAKATI WA STADI ZA KKK NA USAWA WA KIJINSIA
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Shirika la Room to Read zimesaini hati ya makubaliano ya kwa kuendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali yenye lengo la kuboresha elimu nchini kwenye maeneo Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu pamoja na Programu ya Usawa wa Kijinsia.
Akizungumza kwenye hafla ya makubaliano hayo Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Taasisi ya Room to read wamekuwa wakishirikiana nao katika program mbalimbali zenye kuboresha elimu nchini hivyo kwa kusaini makuabaliano haya yatazidisha ushirikiano zaidi, hasa katika suala la kuondoa tatizo la kutojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na kuzingatia usawa wa kijinsia kama ilivyoelekezwa katika dira ya maendeleo ya mwaka 2050.
“TET na Room to Read tutashirikiana katika uandaaji, kupitia na kuhuisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili viendane na viwango vya Mitaala ya Taifa, kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, na Mwongozo wa Kitaifa wa Mitaala ya Elimu Msingi, kwa lengo la kuimarisha ubora na ufanisi wa ujifunzaji wa stadi za msingi,” amesema Dkt. Komba.
Pia, aliongeza kuwa ushirikiano huo utahusisha kuimarisha umahiri wa walimu kupitia mifumo ya mafunzo ya ualimu kabla ya kuanza kazi na mafunzo endelevu kwa walimu walio kazini, kwa kuandaa na kutekeleza mafunzo kwa kuzingatia Mkakati wa Taifa wa Maendeleo na Usimamizi wa Walimu pamoja na vipaumbele vya kitaifa vya kuimarisha umahiri wa walimu na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji darasani pamoja na kuwezesha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa na bila ubaguzi, kwa kuzingatia mahitaji ya kijinsia kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia pamoja na vipaumbele vya elimu jumuishi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Room to Read, Bi.Joan Minja amesema kuwa, ushirikiano huo unajenga msingi rasmi wa kuendeleza, kuimarisha na kupanua ushirikiano katika maeneo muhimu katika kuboresha elimu nchini.
"Tunashukuru kwa nafasi hii ya kuendelea kushrikiana zaidi na kuwa tuna dhamira ya kuwa na uwajibikaji kwa kuzingatia uwazi na kuheshimu taratibu zote za kiserekali na kuwa na ushrikiano wa kitaalamu zaidi kwa kuzingatia matokeo chanya,”amesema Bi. Minja.