Wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu watoa maoni ya Mtaala wa Ualimu
Imewekwa: 23rd September, 2022
Kamati ya Kitaifa ya Uboreshaji Mitaala iliyoteuliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Adolf Mkenda pamoja na Wakuza Mitaala wa Taaasisi ya Elimu Tanzania (TET) wamepata nafasi ya kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa Wakufunzi wa Vyuo Ualimu Kanda ya Mashariki kuhusiana na mapendekezo ya maboresho ya Mitaala ya Elimu ya Ualimu.
Katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 21/9/2022 Mjini Morogoro , Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Makenya Maboko aliwasilisha mapendekezo ya muundo wa elimu ya ualimu na mabadiliko ya mtaala yanayopendekezwa ambapo amesema kuwa, wakufunzi hao wana nafasi ya kutoa maoni yao kwa kamati na itayapokea na kuyafanyia kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amewashukuru wakufunzi hao kwa muda wao wa kushiriki kwenye utoaji wa maoni huku akiwasilisha wasilisho juu ya matokeo muhimu kutoka kwenye taarifa ya uchambuzi wa maoni ya wadau kuhusu elimu ya ualimu.
Dkt. Komba ameeleza kuwa maboresho ya mitaala yanayofanyika ni ya sita tangu nchi ipate uhuru na ameeleza kuwa maboresho hayo ni makubwa yenye lengo la kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwa na wahitimu wenye ujuzi wa kujiajiri, kuajiriwa na kumudu maisha yao ya siku kwa siku.