WIZARA YAJADILI RASIMU YA MABORESHO YA MITAALA
Imewekwa: 06th June, 2022
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
mnamo, Juni 2, 2022 imejadili rasimu ya maboresho ya mitaala
iliyotokana na maoni ya wadau mbalimbali juu ya uboreshaji wa mitaala ya elimu
nchini ikiwa ni maandalizi ya Kongamano la Elimu la siku tatu la kukusanya maoni
ya wadau.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Eliamani Sedoyeka alisema kuwa lengo kubwa la uboreshaji huo
wa mitaala ni kutekeleza maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwamba mitaala ya elimu ilenge kuwaandaa
vijana wa Kitanzania wenye ujuzi, uwezo wa kuzalisha mali na kujitegemea baada
ya kumaliza ngazi yoyote ya elimu.
Mkutano huo uliofanyika Jijini Dodoma,
uliwashirikisha Wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliyowakilishwa na Katibu Mkuu Ally
Khamis Juma, Ofisi ya Rais TAMISEMI iliyowakilishwa na Naibu Katibu Mkuu Elimu,
Dkt. Charles Msonde.
Washiriki wengine ni Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Watoto na Makundi Maalumu iliyowakilishwa na Amon Mpanju,
Naibu Katibu Mkuu, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) iliyowakilishwa na
Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Aneth Komba, Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ)
iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mkuu Bwana. Abdallah Mohamed Mussa na Kamati
ya Kitaifa ya Mitaala iliyowakilishwa na Prof. Makenya Maboko.