Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ni taasisi ya Umma ndani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa na jukumu kuu la kutafsiri sera ya elimu nchini na kuziweka katika mitaala na program za vifaa vya kujifunzia kwa lengo la kutoa elimu bora katika ngazi za elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. TET ilianzishwa kwa sheria Na. 13 ya mwaka 1963 na kuitwa Taasisi ya Elimu kikiwa kitengo ndani ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam chenye jukumu kuu la kuratibu kazi ya utoaji wa mafunzo ya ualimu katika Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na jitahada za Wizara ya Elimu katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji mashuleni na vyuo vya ualimu. Julai 1970, Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam kilipopandishwa hadhi kuwa chuo kikuu kinachojitegemea, Taasisi ya Elimu iliendelea kuwa Kitengo ndani ya chuo hicho hadi mwaka 1975, ilipohamishiwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ikiwa ni taasisi inayojitegemea iliyoundwa kwa sheria ya Bunge Na. 13 ya mwaka 1975. Mwaka 1987, mabadiliko ya sheria Na. 4 yaliibadilisha Taasisi ya Elimu kuwa Taasisi ya Ukuzaji Mitaala bila kubadilishwa jukumu lake la msingi. Hii ilitokana na taasisi kujishughulisha na kazi ya kubuni na kukuza mitaala ya ngazi mbalimbali za elimu. Taasisi ilibadilishwa jina na kuitwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa sheria ya Bunge No. 5 ya mwaka 1993. Mabadiliko haya yalitokana na jina la awali la Taasisi ya Ukuzaji Mitaala kutoakisi wajibu mpana wa taasisi. Julai 2009 TET ilipewa hadhi ya kuwa taasisi ya elimu ya juu isiyokuwa Chuo kikuu inayotoa mafunzo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania – NACTE ikiwa na jukumu la kutoa mafunzo katika fani ya Ubunifu na Ukuzaji Mitaala. Majukumu ya msingi ya TET ni:
- Kubuni na kukuza Mitaala katika ngazi za elimu ya awali, elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu
- Kutoa mafunzo kwa walimu tarajali na walio kazini ili kuleta ufanisi na matokeo bora ya utekelezaji wa mitaala
- .Kutoa na kuhakiki uthibiti wa ubora wa elimu unaohusu mbinu za ufundishaji, malengo ya masomo na viwango vya zana za kufundishia na kujifunzia
- Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa serikali kupitia Wizara na wadau wa elimu unaolenga kuboresha elimu katika ngazi mbalimbali.
|