Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Elimu Tanzania

MEWAKA NI TEGEMEO KUBWA KATIKA UJIFUNZAJI NA UFUNDISHAJI - DKT. KOMBA

Imewekwa: 30 March, 2026
MEWAKA NI TEGEMEO KUBWA KATIKA UJIFUNZAJI NA UFUNDISHAJI - DKT. KOMBA
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Mpango wa mafunzo endelevu kazini (MEWAKA) ni moja ya mkakati muhimu katika Sekta ya Elimu unaosaidia kuboresha ujif

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema kuwa Mpango wa mafunzo endelevu kazini (MEWAKA) ni moja ya mkakati muhimu katika Sekta ya Elimu unaosaidia kuboresha ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu na wanafunzi nchini.

Dkt. Komba amesema hilo leo Machi 30, 2026 Mkoani Morogoro alipofungua kikao cha uhakiki wa matini ya uendeshaji wa jumuiya za kujifunza kwa walimu na viongozi wa elimu kilichoshirikisha wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ADEM, TET na wadau kutoka Shule Bora. 

Amesema, Serikali imeendelea kutekeleza Mtaala ulioboreshwa tangu Januari 2024, hivyo kuendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na MEWAKA na Jumuiya za ujifunzaji imara ili kuchochea utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa kwa ufanisi unaotakiwa.

"Unapokuwa na MEWAKA imara pamoja na Jumuiya za ufundishaji imara inakupa uhakika walimu wanaujuzi unaostahili kulingana na wakati na wanaweza kutekeleza Mtaala ulioboreshwa kwa ufanisi." Amesema Dkt. Komba.

Aidha, Dkt. Komba ameipongeza ADEM kwa kuunganisha matini ya uendeshaji wa jumuiya za kujifunza kwa walimu na viongozi wa elimu, kwani utasaidia kuongeza kasi ya utendaji na utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa kupitia MEWAKA, na Jumuiya za ujifunzaji.

Kwa upande wake  Mtendaji Mkuu ADEM Dkt. maulid J. Maulid ameeleza kuwa, umuhimu mkubwa wa uanzishwaji wa jumuiya za kujifunza ni kubadilishana uzoefu na maarifa ya kitaaluma,  huku akisisitiza kwasasa MEWAKA imetanua utendaji wake kutoka kwa walimu mpaka kwa viongozi wa elimu wakiwemo walimu wakuu na maafisa elimu kata ili kuchochea ufundishaji na ujifunzaji. 

Nae, Mwakilishi kutoka Shule Bora Bw. Isuja Silvester ameipongeza Serikali kwa namna inayoendelea kusimamia uboreshaji wa elimu nchini hasa kupitia jumuiya za ujifunzaji na MEWAKA hali inayochochea ufanisi katika utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa nchini ulioanza Januari 2024.

Sambamba na hilo amesema, Mradi wa shule Bora utaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha lengo la kuboresha Elimu kwa ufanisi linafikiwa.

Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania