WALIMU WA SOMO LA BIASHARA WAASWA KUWAANDAA WANAFUNZI KWA VITENDO ILI WAPATE UJUZI WA KIWEZA KUJITEGEMEA
Naibu Katibu Mkuu (elimu) Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw. Atupele Mwambene amewataka walimu waliopata mafunzo ya somo la biashara kwenda kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo maarifa waliyopata katika mafunzo hayo ili kupata wahitimu wenye kutambua fursa zitakazowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Ameyasema hayo leo tarehe 29/07/2026 wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya walimu wa ajira mpya wa somo la Elimu ya Biashara yaliyofanyika katika chuo cha Ualimu Morogoro.
"Hapa walimu nawaomba sana mkawafundishe wanafunzi kwa vitendo zaidi tuachane na nadharia ili tupate wabunifu, wazalishaji, wafanyakazi na wajasiriamali wenye tija na baadae waweze kuajiri wenzao na kufikia dira ya maendeleo yetu yenye tija ya mwaka 2050.” Amesema Bw. Mwambene.
Ameongeza kwa kuwataka walimu kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata maadili na tataribu za Serikali pamoja kutumia teknolojia kwa usahihi ili kuwasaidia katika eneo lao la fundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema kuwa mafunzo hayo yamendelea kuwa tija katika kuwapa walimu maarifa yatakayowasaidia katika kupata mbinu mbalimbali zitakazowasaidia katika eneo la Ufundishaji na Ujifunzaji na kuwaomba walimu hao kuhakikisha wanatumia vyema maarifa waliyoyapata.
Naye, Mwakilishi wa EDUCATE Bw. Neilson Musikila amesema fursa waliyoapata ya kuchangia katika kuboresha elimu kwao ni jambo kubwa ambalo wataendelea kuliunga mkono ili kuhakikisha walimu husika wanaendelea kupatiwa maarifa yatakayowasaidia katika kutekeleza kazi zao vyema.
Mwakilishi wa walimu waliopatiwa mafunzo, Bw. Chrilis Salapion ameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo yatakayowawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi baada ya kupata maarifa mapya.
Jumla walimu 702 wa somo la Elimu ya Biashara kutoka shule za Serikali za Serikali wanashiriki mafunzo hayo ambapo mafunzo yaliyopita jumla ya walimu 1965 walipatiwa mafunzo ya aina hiyo ambapo yanatolewa na wataalamu kutoka TET pamoja na vyuo vya ualimu.