Watumishi wa TET watakiwa kufanya kazi kwa Uadilifu.
Imewekwa: 13th July, 2022
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Dkt.Francis Michael amewataka watumishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kufanya kazi kwa weledi ,nidhamu katika kuhakikisha suala la elimu linaendelea kuimarika nchini.
Dkt.Michael ameyasema hayo tarehe 11/7/2022 jijini Dar es salaam katika ziara yake ya siku moja kwenye makao makuu ya TET ambapo amesema kuwa Serikali inawategemea katika kazi kubwa ya masuala ya elimu.
"Nawaomba mfanye kazi kwa weledi na kuhakikisha suala la elimu na haswa haya maboresho ya mitaala yanayoendelea yafanyike vizuri,alisema Dkt.Michael.
Pia Dkt.Michael amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu kwa namna anavyoendelea kuwajali watumishi wa umma kutokana na nyongeza za mishahara na kuwataka watumishi wa TET kutomwangusha Rais ,na badala yale wafanye kazi ipasavyo.
Kabla ya kufanya kikao na watumishi wote,Dkt.Michael alipata nafasi ya kufanya kikao na Menejimenti ya TET na kufahamu masuala mbalimbali .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt.Aneth Komba amesema kuwa wameshukuru ujio wa Katibu Mkuu na kuwa TET inaendelea kufanya kazi zake katika kuzingatia misingi ya kiutumishi na kuwa suala la maboresho ya mitaala linaloendelea litafanyika vizuri.
Katibu Mkuu katika ziara yake aliambatana na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Bwana.Moshi Kabengwe.