TET NA SILOAM KUSHIRIKIANA KUANDAA VITABU VYA BRELI
Imewekwa: 08th June, 2022
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) tarehe 06/06/2022 ilifanya mazungumzo na Shirika la Siloam Center for the Blind la nchini Korea.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za TET zilizopo Jijini Dar es salaam ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano na kukubaliana kuandaa vitabu vya Breli kwa ajili ya wanafunzi wasioona wa ngazi zote za elimu nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Siloam Center for the Blind Bwana Dong ic Choi ameahidi kuwa kwa mwaka huu wa fedha shirika hilo litachapa vitabu katika maandishi ya Breli kwa vitabu vyote vya Kiada vya Ngazi ya Elimu ya Sekondari vitakavyoandaliwa na TET.
Katika ushirikiano huu Siloam watazalisha vitabu Nchini Korea kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuvisafirisha mpaka Tanzania, ambapo TET itafanya jukumu la kuvitoa bandarini na kuvisambaza katika shule husika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TET Dkt.Aneth Komba ameshukuru na kuahidi kuwa ,Taasisi itatimiza majukumu yake kwa wakati ili kuhakikisha wanafunzi wasioona wanapata vitabu vya kujifunzia ambayo ni haki yao ya msingi.
Kwa sasa vitabu hivyo hugawiwa kwa uwiano wa vitabu vitatu kwa mwanafunzi mmoja.