Imewekwa: 19th October, 2023
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) tarehe 18/10/2023 wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kikazi wenye lengo la kusaidia kutoa elimu juu ya suala la rushwa katika mitaala na uandishi wa vitabu vya kiada.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba ameeleza kuwa makubaliano hayo ya ushirikiano na TAKUKURU yatajikita katika maeneo saba ambayo ni TAKUKURU kuandaa na kuwasilisha TET maudhui ya masuala mbalimbali yanayohusu kuzuia na kupambana na rushwa ambapo Masuala hayo yatachopekwa kwenye vifaa mbalimbali vya ujifunzaji na ufundishaji, TAKUKURU na TET watatoa mafunzo kwa walimu wa masomo juu ya namna ya kutekeleza mtaala pamoja na kutumia vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinavyokuza uelewa juu ya masuala ya kuzuia na kupinga rushwa.
Maeneo mengine ni TAKUKURU na TET kutoa mafunzo kwa waandishi wa vitabu vya shuleni na waandishi wengine wa maudhui yanayopinga rushwa juu ya namna ya kuingiza masuala ya kupinga rushwa katika maandiko mbalimbali, TAKUKURU na TET kuunda timu ya kutathmini utekelezaji wa mtaala unaozingatia masuala ya kupinga rushwa.
Pia ushirikiano utakuwepo katika kubadilishana taarifa ili kuzuia rushwa katika hatua za uandaaji wa mitaala na kwamba TAKUKURU na TET watafanya shughuli nyingine zozote zenye maslahi ya pamoja kadiri ya makubaliano ya pande zote mbili
“Ninaamini kuwa kupitia ushirikiano huu tutaweza kuwafikia wanafunzi na walimu ambao tunatarajia watasaidia kuiambukiza jamii kwa ujumla kuwa na tabia njema, maadili mema na tabia ya kuzuia, kupinga na kuikataa rushwa na kuwa kupitia ushirikiano huu jamii itapata uelewa na mambo mbalimbali yahusianayo na rushwa na tutajenga kizazi chenye maadili na kinachokataa na kupinga rushwa” amesema Dkt. Komba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni amesema kuwa makubaliano kati yao na TET yatasaidia sana katika kuchangia utoaji wa elimu dhidi ya rushwa nchini kwani vijana kuanzia ngazi ya elimu ya chini wataweza kupata uelewa kuhusu rushwa na madhara yake na hivyo kuikataa rushwa .
“Ni jambo jema sana hili kwani tutaanza kuwapandikizia tokea wanafunzi wakiwa na umri mdogo kupata uelewa juu ya masuala ya rushwa na kufanya wakue wakiwa na maadili mema”amesema Hamduni.
CP Hamduni amesema kuwa makubaliano hayo yataendeleza juhudi za utoaji elimu kwa jamii na hususan vijana Klabu za Wapinga rushwa na kuwa hadi kufikia Juni 2023, wameweza kuanzisha klabu 10,736 zenye wanachama 1,091,439 katika Shule za Msingi,sekondari na katika Vyuo na Taasisi za Elimu ya Juu nchini.
Kamishna Hamduni pia amewaomba wadau wakiwemo vyombo vya habari kushirikiana na Serikali katika kuzuia rushwa kwa kuunga mkono kaulimbiu ya TAKUKURU isemayo KUZUIA RUSHWA NI JUKUMU LAKO NA LANGU; TUTIMIZE WAJIBU WETU.