Imewekwa: 14th May, 2022
RASIMU YA MTAALA YAANZA KUANDIKWA
Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania
(TET) imeanza kazi ya uandishi wa rasimu za mitaala ya elimu ya Awali, Msingi,
Sekondari na Ualimu.
Akifungua kikao kazi cha uandishi wa rasimu hivi karibuni katika chuo cha Veta
Jijini Dodoma ambapo mwenyekiti wa kamati ya Kitaifa ya uboreshaji wa Mitaala
Prof. Makenya Maboko amesema kuwa kazi hiyo ni muhimu kwa maslahi ya taifa na
kuwataka wataalam mbalimbali kutumia nafasi hiyo kuifanya kwa weledi mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Elimu Tanzania (TET) amesema Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kupitia
TET imekamilisha zoezi la kuchakata maoni ya wadau juu ya hali ilivyo sasa ya
mitaala ya elimu nchini, hatua inayofuata sasa ni kuandaa rasimu za mitaala
hiyo.
Amesema kuwa rasimu zitakazoandaliwa ni rasimu ya Mitaala ya Elimu ya Malezi,
Awali, Msingi, Sekondari, Sekondari ya juu na Ualimu.
Aidha amewataka wataalamu mbalimbali wanaoshiriki katika kazi hiyo ya uandishi
kuifanya kazi kwa kuangalia maslahi ya taifa kwa kuwa Serikali inahitaji
mageuzi makubwa kwenye elimu.
" Mmeaminiwa kuisaidia Serikali katika kuleta mageuzi kwenye Elimu, maoni
ya wadau ni kuwa Mitaala imejaa vitu vingi visivyo na msaada kwa watoto,
ninawaomba muangalie vitu vitakavyowasaidia kulingana na karne tuliyopo"
amesema Dkt. Komba
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ubunifu na Ukuzaji wa Mitaala Dkt.
Godson Lema amesema kuwa, kazi hiyo inawashirikisha wataalam kutoka vyuo vikuu
Tanzania Bara na Zanzibar, Wataalamu kutoka VETA, vyuo vya ualimu, vyuo vya
ufundi, wadhibiti ubora, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wataalamu
kutoka wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, walimu
kutoka shule za msingi na sekondari pamoja na wakuza mitaala kutoka TET.