Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Elimu Tanzania

WADAU WAOMBWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KAMPENI YA KITABU KIMOJA, MWANAFUNZI MMOJA

Imewekwa: 12 March, 2025
WADAU WAOMBWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KAMPENI YA KITABU KIMOJA, MWANAFUNZI MMOJA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja ili kuchoche

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja ili kuchochea maendeleo katika Sekta ya Elimu nchini.

Ametoa wito huo, leo Machi 7, katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ulioambatana na matembezi ya hisani ya kuhamasisha upatanikaji wa fedha utaosaidia kufikia lengo la kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja katika ofisi ya TET, jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo, ametoa rai kwa uongozi wa taasisi hiyo kuongeza wigo wa kuimarisha upatikanaji wa vitabu kwa kushirikisha kampuni za uchapishaji na wadau wa Sekta binafsi ili kupunguza gharama za uchapishaji.

"Ushiriki wa wadau katika uchapishaji wa vitabu utasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa vitabu shuleni, na kufikia lengo la kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. “Vitabu ni chanzo cha maarifa na maendeleo, na ni muhimu katika kuhakikisha elimu bora kwa wanafunzi.” Amesema.

Aidha, Mhe. Majaliwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa aliyoyafanya katika Sekta ya elimu nchini, ikiwemo uboreshaji wa Mitaala inayoendana na mahitaji ya sasa ya Sayansi na Teknolojia, ajira kwa walimu pamoja upatikanaji wa vitabu vya kujifunzia na kufundishia.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba alisema maadhimisho ya miaka 50 TET pamoja na kampeni ya kitabu kimoja mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu, huku lengo likiwa kukusanya Bilioni 297 zitazosaidia kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na kitabu chake.

“Maadhimisho haya yanalenga kukusanya shilingi bilioni 297 kwa ajili ya kufikia azma ya kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja na ununuzi wa kompyuta za kuhifadhi vitabu.”Amesema Dkt. Komba.

Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania