PLAY MATTERS WATEMBELEA TET
Imewekwa: 19th August, 2023
PLAY MATTERS WATEMBELEA TET
Shirika lisilo la Kiserikali PlayMatters lililoanzishwa mwaka 2020 katika nchi za Uganda,Ethiopia na Tanzania kwa ajili ya mpango wa ufundishaji na ujifunzaji kupitia michezo shuleni leo tarehe 17/08/2023 limetembelea Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA).
Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TET Jijini Dar es salaam,Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema kuwa,TET inashirikiana na PlayMatters katika kuwapa mafunzo walimu waliopo makazini. Aidha,amasema shirika hilo limeandaa Matini yenye maudhui ambayo yatawasaidia walimu kuwajengea uwezo juu ya namna ya kutumia michezo katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji
"Kama mnavyojua, Serikali ya awamu ya sita inafanya mapitio makubwa ya mitaala na katika rasimu za Mitaala tunazozipendekeza tumependekeza na kusisitiza matumizi makubwa ya michezo katika ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto. Hivyo PlayMatters wamekuja wakati muafaka na tutashirikiana nao ipasavyo katika kuhakikisha kwamba hii mbinu ya kutumia michezo inawafikia walimu wote na wanaweza kutumia vizuri kuwafanya watoto waweze kujifunza.Naamini njia hii ikitumiwa vizuri hatuwezi kupata mtoto anayefika darasa la pili akiwa hawezi kusoma,kuandika na kuhesabu" amesema Dkt Aneth.
Kwa upande wa wawakilishi kutoka Wizara ya Elimu Uganda na Ethiopia, wameipongeza TET kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha walimu wote nchini wanapata mafunzo kazini kwa kutumia teknolojia ambayo ni njia rahisi kufikiwa na walimu wote.
Awali, Mkuza Mtaala Bwana Onesmo Sedikia aliwasilisha wageni hao jinsi mfumo wa Learning Managent System (LMS) na Online library unavyotumiwa na walimu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji ikiwa ni pamoja na kujiendeleza kitaaluma.
Wageni hao wametoka Wizara ya Elimu ya Uganda, Ethiopia, na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais -TAMISEMI.