DURU YA NNE YA TUZO YA TAIFA YA MWL. NYERERE YA UANDISHI BUNIFU YAZINDULIWA

Duru ya nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025/2026 imezinduliwa leo tarehe 06/08/2025 Jijini Dar es salaam ambapo Waandishi Bunifu nchini wameombwa kujiandaa kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya kushindanishwa .
Akitangaza mbele ya waandishi wa Habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa ni muda sasa kwa Waandishi Bunifu nchini kuwasilisha kazi zao kwa kamati ya Kitaifa ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa lengo la kukuza uandishi na lugha ya Kiswahili nchini.
"Muda umefika sasa wa waandishi kuwasilisha kazi zao bunifu ili ziweze kushindanishwa, hivyo, nawaomba wadau mjitokeze kwa wingi kuwasilisha kazi zenu" amesema Prof. Mkenda.
Pia, Prof. Mkenda aliwaeleza waandishi kuwa awali kilifanyika kikao kilichowahusisha wadau wa Uandishi Bunifu kwa ajili ya kuzungumza namna ya uboreshaji wa tuzo hizo ili ziendelee kuwa bora na zenye kuleta tija ya uchocheaji wa usomaji vitabu na kukuza lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, amesema kuwa miswada hiyo itahusisha nyanja ya Riwaya, Tamthiliya, Ushairi na Hadithi za Watoto kama ilivyokuwa mwaka 2024/2025. Aidha, ameendelea kusema kuwa miswada hiyo itaanza kupokelewa Agosti 15, mwaka huu hadi Novemba 30. Vilevile, Prof. Mlama amewaomba Waandishi Bunifu kujitokeza kwa wingi katika kuwasilisha miswada.
"Nawakaribisha wadau wote wa Uandishi Bunifu wa rika zote popote mlipo muweze kuleta miswada yenu ishindanishwe na tuna imani mwaka huu mtajitokeza wengi zaidi " amesema Prof. Mlama.
Pia, Prof. Mlama ameongeza kuwa, baada ya zoezi hilo la upokeaji kukamilika majaji wataanza kazi ya kupitia miswada yote na hafla ya kuwatangaza washindi itafanyika tarehe 13/04/2026 ikiwa ni kumbukizi ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kamabarage Nyerere.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amewashukuru wadau wote wa Uandishi Bunifu walioshiriki kikao cha mazungumzo yenye lengo la kuboresha tuzo hiyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali na wadau wa Uandishi Bunifu nchini ambao wametoa maoni mbalimbali yenye lengo la kuboresha Tuzo hiyo.