Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Elimu Tanzania

WAZIRI MKUU AFARIJIKA NA JITIHADA ZA TET ZA UKUSANYAJI MICHANGO ILI KUFANIKISHA KAMPENI YA KITABU KIMOJA, MWANAFUNZI MMOJA.

Imewekwa: 17 June, 2025
WAZIRI MKUU AFARIJIKA NA JITIHADA ZA TET ZA UKUSANYAJI MICHANGO ILI KUFANIKISHA KAMPENI YA KITABU KIMOJA, MWANAFUNZI MMOJA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefarijika na jitihada zinazoendelea za ukusanyaji wa michango ili kufanikisha kampeni ya Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amefarijika na jitihada zinazoendelea za ukusanyaji wa michango ili kufanikisha kampeni ya Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja ambapo mpaka sasa Bilioni 2.3 zimeshakusanywa katika malengo ya kukusanya Bilioni 35 katika kipindi cha miaka mitano. 

Amesema hayo leo Juni 17, 2025 katika ofisi za TET Jijini Dar es Salaam wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania.

"Nimefarijika kusikia kuwa shilingi bilioni 2.3 zimeshakusanywa katika malengo ya Kampeni ya kukusanya shilingi bilioni 35 katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2026-2031."

Amesema, taasisi hii ni moyo wa elimu nchini na hasa kwa kuwa ndiyo inayojenga msingi wa elimu kuanzia Darasa la Awali mpaka Kidato cha Sita. Kutokana na ukweli huo, serikali itaendelea kuiimarisha ili ifikie maono ya kuwa kitovu-Maridhawa cha ubora katika uandaaji, ukuzaji na ubunifu wa mitaala. 

Sambamba na hilo Mhe. Majaliwa ametoa rai kwa kampuni nyingine za simu kufikiria kuondoa gharama katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA ya kujifunzia kama walivofanya kampuni ya AIRTEL ili kufanikisha matumizi ya mifumo hii ya kidigital kwa walimu na wanafunzi bila gharama.   

Aidha, Mhe. Majaliwa amewapongeza wadau wote walioshiriki na watakaoendelea kushiriki kufanikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa kampeni ya "Kitabu kimoja, Mwanafunzi  mmoja", huku akionesha kuwatambua wadau waliokubali kuhamasisha na kuchangia kampeni hii ikiwemo wale wanaochangia kupitia kampeni ya elimu ya fedha yaani financial literacy na utalii. 

Pia, Mhe. Majaliwa ametoa wito kwa mashirika, taasisi, vikundi mbalimbali na mtu mmoja moja kuendelea kuiunga mkono kampeni ya "Kitabu kimoja, Mwanafunzi mmoja" ili kufikia lengo ndani  ya muda, huku akisisitiza kampeni  hiyo inaenda na ukusanyaji wa kompyuta mpakato maalumu moja kwa mwanafunzi mmoja kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.

Pamoja na hayo, amesema Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa fedha za vitabu kwa kutoa fedha za ruzuku za wanafunzi yaani capitation grants zinazotolewa moja kwa moja TET kupitia Wizara ya Elimu.

Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu Tanzania