Imewekwa: 09th December, 2021
Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeiagiza
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha wataalamu wake wanapata
nafasi ya kujifunza uzoefu kutoka nchi
nyingine utakaowawezesha katika kufanya
maboresho ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Kamishna wa Elimu nchini, Bwana Venance Manori ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo katika mkutano wa kupeana uzoefu katika
uboreshaji wa mitaala unaofanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa Hazina kuanzia tarehe 8 hadi 9/12/2021.
Amesema
majadiliano ya uzoefu wa kuboresha mitaala kwa nchi nyingine yatawezesha
wataalamu wa hapa nchini kufanya kazi
hiyo kwa weledi.
“Naamini
mtatumia fursa hii adhimu ya uzoefu wa
nchi nyingine kwa ajili ya kupata ujuzi
wa kuendelea na kazi ya maboresho ya mitaala iliyoanza hapa nchini,"
amesema Akwilapo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema mkutano huu una lengo la kuwajengea
uzoefu wakuza mitaala juu ya namna nzuri ya kufanya kazi ya mapitio ya mitaala.
“Kazi
ya maboresho inaendelea kwa sasa iko katika hatua ya kupata maoni kwa wadau
mbalimbali nchini, hivyo uzoefu wa nchi nyingine utatuwezesha kupata uelewa
mpana katika kazi hii ya maboresho ya
mitaala," amesema Dkt. Komba
Kwa
upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sekondari, kutoka Ofisi ya
Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bi Khadija Mcheka amesema,
majadaliano hayo ya kupata uzoefu wa kuboresha mitaala kwa nchi nyingine yatasaidia sana katika kupata
elimu iliyo bora nchini hasa katika zoezi la uboreshaji mitaala linaloendelea.
TET
imefanikiwa kupata uzoefu wa uboreshaji mitaala ya elimu kutoka nchini Kenya
ambayo ilitumia muda wa miaka mitano katika kufanya maboresho yao,ambapo kwa Tanzania
zoezi la uboreshaji Mitaala linatarajiwa kutumia miaka minne .