TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU YAZINDULIWA RASMI
Imewekwa: 21st September, 2022
TUZO YA TAIFA YA MWALIMU NYERERE YA UANDISHI BUNIFU YAZINDULIWA RASMI
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof.Adolf Mkenda(Mb) amezindua tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu yenye lengo la kukuza sekta ya uandishi, uchapishaji na usambazaji wa vitabu nchini. Aidha, tuzo hiyo inalenga kukuza ari ya usomaji nchini
Halfa hiyo ya uzinduzi imefanyika katika ukumbi wa Auditorium uliopo katika Jengo la makao makuu ya Benki ya CRDB Jijini Dar es salaam.
Prof.Mkenda amesema kuwa kutokana na tabia ya usomaji wa vitabu kuendelea kupungua uandishi bunifu nao unaendelea kupungua.Hivyo, lengo lingine la kuanzisha tuzo hii ni kufungua ukurasa mpya wa kuchochea uandishi, uchapishaji na usambazaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati teule ya tuzo Prof.Penina Mlama amasema kuwa uandishi bunifu ni moja ya tunu adhimu ya Taifa lolote.
Pia ameongeza kua tuzo hiyo imepewa jina la Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye pia alikuwa mwandishi wa mashairi na mfasiri wa tamthiliya. Sababu ni nyingine ni kuwa Mwl. alikuwa kiongozi aliyekuza mawazo huru na kuchochea kwa kiwango kikubwa kukua kwa lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa na Kimataifa.
Aidha ameeleza kuwa kwa Mwaka huu wa Fedha waandishi wa kazi bunifu watashindana katika nyanja mbili ambazo ni Riwaya na Tamthilia.
Vilevile, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa, Dirisha la kupokea miswada litakuwa wazi kuanzia tarehe 13 Septemba hadi tarehe 30 Novemba 2022 na kuwa Miswada itapokelewa kupitia barua pepe tu kwa anuani tuzonyerere@tie.go.tz.