KAMATI YA USTAWI WA JAMII YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA TET
Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Husein Ibrahim Makungu amewaongoza wajumbe wa Kamati hiyo kwenye ziara ya kikazi katika ofisi za Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) jijini Dar es salaam leo tarehe 28/04/2026. Mwenyekiti huyoa ameeleza kuwa ziara hiyo imewawezesha kujifunza na kupata uzoefu juu ya kazi zinozofanywa na TET. Pia, ameeleza kuwa wajumbe wa Kamati wamepata wakati mzuri wa kusikia mawasilisho mbalimbali yaliyohusu maboresho ya elimu nchini na kueleza kuwa ni nafasi pekee kwao kuchukua uzoefu walioupata kutokana kazi nzuri inayofanywa TET na kuwaasilisha katika Vikao vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
“Tumepata nafasi ya kujifunza kwa kweli, mawasilisho ni mazuri yenye maarifa makubwa hasa katika uboreshaji wa elimu nchini “alisema Mhe. Makungu.
Vilevile, Mhe. Makungu alisema kuwa wameweza kusikia mawasilisho juu ya maboresho ya mitaala yaliyofanyika na utekelezaji wake unavyoendelea kwa sasa nchini.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar Mhe. Khadija Salum Ally alisema kuwa yeye na wajumbe wengine waweza kujifunza na kufahamu masuala mbalimbali ya maboresho ya elimu na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa upande wa mwakilishi wa Kamishna wa Elimu nchini, Bw.Victor Bwindiki akitoa salamu za Kamishna wa Elimu, alisema kuwa ugeni huo una maana kubwa katika kukuza ushirikiano wa masuala ya Elimu nchini.Hivyo, ni jambo jema lililofanyika kwa wajumbe hao kupata nafasi ya kutembelea TET.
Naye , Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania , Dkt. Aneth Komba alishukuru wajumbe hao kuichagua TET kwenye ziara yao ya kikazi na kuwa wamechukua maoni waliyopatiwa na wawakilishi hao kwa ajili ya kuyafanyia kazi.
Katika ziara hiyo wajumbe wa Baraza la Wawikilishi walipata nafasi ya kujadiliana na menejimenti ya TET kwa lengo la kuboresha elimu.