Vitabu vya kiada,baadhi vya ziada na machapisho mbalimbali ya kielimu yapatikana bure katika maktaba mtandao ya TET
Imewekwa: 06th June, 2023
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inajivunia matumizi ya teknolojia kwa sasa ambapo vitabu vyote vya kiada, baadhi ya vitabu vya ziada na machapisho mbalimbali yanapatikana katika tovuti ya TET kupitia maktaba mtandao ambapo kwa sasa ni rahisi kwa mtu yoyote kuweza kuvipata na kusoma kwa urahisi.
Hayo yasemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt.Aneth Komba katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi hivi karibuni katika makao makuu ya TET jijini Dar es Salaam.
“Kwa sasa ukiwa na laini ya airtel unaweza kuingia na kusoma bila kuwa na data (internet) tunaendelea kuzungumza na wadau wengine wa mitandao mbalimbali kuhakikisha machapisho yanapatikana bure ili kuwezesha usomaji kuwa rahisi kwa mtu yoyote atakayehitaji”amesema Dkt.Komba.
Pia, ameeleza kuwa teknolojia imesaidia katika upande wa mafunzo ya walimu kazini kwa kutumia mfumo maalumu ulioandaliwa kwa ajili ya kuwafundisha walimu kupitia Jumuiya za Ujifunzaji ambapo katika mfumo huo zaidi ya walimu 100,000 huingia kila siku na kuweza kuwasiliana na wataalamu wa TET.
Ameongeza kuwa, mfumo huo umeweza kupunguza gharama za kuwakusanya walimu katika eneo moja kwa ajili ya kuwapa mafunzo kazini.