TEKNOLOJIA YA AI KATIKA VITABU VYA KUFUNDISHIA KUSAIDIA ELIMU JUMUISHI.
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba amesema Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kuja na mfumo wa vitabu vya kufundishia vinavyotumia akili mnemba (AI) itayosaidia Elimu jumuishi katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi nchini.
Ameyasema hayo Julai 27, 2026 wakati akifungua kikao kazi cha siku sita cha kubadili maudhui kutoka kwenye nakala ngumu kwenda kwenye mfumo utaosaidia matumizi ya AI ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wote ikiwemo wenye mahitaji maalumu.
Amesema, kupitia ushirikiano wa Taasisi ya Elimu Tanzania na UNICEF hakuna mtoto wa Tanzania ataeachwa kwani mpango huu utasaidia ujifunzaji na ufundishaji kwa watoto wote, wakiwemo wenye mahitaji maalumu.
Aidha, Dkt. Komba ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza mazingira mazuri ya ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuboresha Elimu nchini.
Naye, Meneja wa Elimu kutoka UNICEF Bw. Ayubu Kafyulilo amesema, mpango huu ni shirikishi umelenga kuviongezea uwezo vitabu kuwa jumuishi ili kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu katika ujifunzaji na ufundishaji.
Amesema, vitabu hivi vitakua na mfumo wa lugha ya alama na vitakua na viambata vya sauti ambavyo vitasaidia mtoto mwenye ulemavu wa uoni, na kwa mwenye ulemavu wa kusikia vitamsaidia kupitia lugha ya alama itayokuwepo katika vitabu hivyo.