MABADILIKO YA MTAALA HUMSAIDIA MWANAFUNZI KUMALIZA NA UJUZI UTAOMSAIDIA KUJIAJIRI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema mabadiliko ya Mitaala barani Afrika humsaidia mwanafuzi kupata ujuzi baada ya kumaliza masomo yake ambao utamuwezesha kujiajiri ama kuajijiriwa.
Pro.Shemdoe ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam akiwa ni mgeni rasmi katika mkutano wa sita ambao unahusisha wataalamu mbalimbali wa Elimu unaofanyika kwa siku nne kuanzia tarehe 22 - 25 Septemba katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa JNICC jijini Dar es salaam.
Prof.Shemdoe amesema mabadiliko ya Mitaala Afrika yamejikita katika ushindani tofauti na ile ya zamani ambapo ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) kuoyesha juhudi katika kuwezesha Tanzania kuwa mwenyeji katika mkutano huo wa sita wa ACA ambao unahudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka nchi 22 duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt Aneth Komba amesema lengo la kukutana katika kongamano la ACA kujadili masuala makuu ya Mitaala ambapo Afrika wana ajenda ya kuandaa Mitaala inayozingatia uafrika na mahitaji ya teknolojia ya sasa.